Thursday 14 December 2017

Wananchi Saranga wavutiwa na huduma za ‘One Stop Centre’




BAADHI ya wananchi wanaoishi Kata ya Saranga eneo la Kimara Temboni jijini Dar es Salaam wamejitokeza kupata huduma za pamoja kwa waathirika kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ‘One Stop Center’.
Huduma hiyo iliyoanza kutolewa Desemba 11 na Kituo cha Usuluhishi –CRC, kilichopo chini ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) imelenga kusogeza karibu na wananchi huduma za msaada wa kisheria kwa waathiriwa wa matukio ya ukatili wa kijinsia pamoja na huduma zingine muhimu kwa kundi hilo.
Huduma zilizotolewa ni pamoja na msaada wa kisheria kwa waathirika wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, Ushauri Unasihi na Dawati la Jinsia linalohudumiwa na Jeshi la Polisi. Wakizungumza baadhi ya wananchi waliopatiwa huduma kituoni hapo walisema wanafurahishwa na huduma hizo muhimu kutolewa eneo moja jambo ambalo linawapunguzia mzigo na urasimu wanapoziitaji.
“Mimi nawashukuru sana waliotuletea huduma hizi (CRC) jirani, hii inatupunguzia mzigo kwa kweli kuna mlolongo mkubwa sana unapozifuatilia maeneo mengine, tungependa zitolewe siku zote kama leo, nadhani vitendo hivi vingepungua,” alisema Ally Mpate akizungumza mara baada ya kupata huduma.
Kwa upande wake Bi. Salome Mlimbo alisema wapo baadhi ya watu wanaishi ndani ya vitendo vya unjanyasaji lakini wanashindwa kujitokeza kutokana na umbali na urasimu uliopo katika kupata huduma hizo, hivyo kushauri zisogezwe jirani na pamoja.
Hivi karibuni Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi –CRC, Bi. Gladness Munuo kilichopo chini ya TAMWA, aliishauri Serikali kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya pamoja kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia ‘One Stop Center’ ili kuwasaidia waathirika wa matukio hayo.



No comments:

Post a Comment

CRC YATOA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI MAKUMBUSHO

Kituo cha usuluhishi na Upatnishi  (Crisis Resolving Center – CRC) kimetoa huduma ya siku mbili inayojulikana kama huduma ya mkono kwa mkono...