Kituo cha Usuluhishi na
Upatanishi (Crisis Resolving Center – CRC) kimetoa huduma ya siku mbili
inayojulikana kama huduma ya mkono kwa mkono au ‘one stope center’. Huduma hii ilianza jana tarehe 12 na
itamalizika leo tarehe 13 ambapo wahanga wa ukatili wa kijinsia wanapatiwa bure huduma za pamoja kutoka kwa Wanasheria, Polisi, Madaktari na Afisa
ustawi wa jamii.
Akitoa tathmini fupi kwa huduma iliyotolewa jana kwa wakazi wa Mwananyamala, Afisa ustawi wa jamii wa kituo cha usuluhishi na upatanishi (CRC) Bi Violeth Chonya alisema, muitikio wa wananchi waliojitokeza kupata huduma
za pamoja ni mkubwa, ambapo jumla ya kesi 31 zilisikilizwa na kufikia
hatua mbalimbali huku kesi 2 za matuzo kwa watoto zikitatuliwa baada ya
kukutanishwa pande mbili za wazazi na kufikia muafaka juu ya mvutano baina yao.
Bi. Violeth alisema kuwa muitikio mkubwa wa wananchi unaonyesha uhitaji mkubwa wa huduma hii kwa jamii huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi leo amabapo hii inaendelea kutolewa kwa siku ya pili na ya mwisho kwa eneo la Mwananyamala.